Alhamisi 10 Aprili 2025 - 14:06
Ikiwa jamii itaishi kwa mujibu wa Qur’ani, adui hataweza kuishambulia

Hawza/ Hadhrat Ayatollah al-Udhma Jawadi Amoli amesisitiza kwamba Qur’ani inapaswa kuwa sehemu hai ya maisha ya Waislamu, na kusema kuwa: "Umma wa kiislamu unapaswa kuwa imara kiasi cha kwamba adui asiwe na ujasiri wa kuushambulia.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatollah Jawadi Amoli, siku ya Jumatano katika darsa lake la Akhlaq liliyofanyika katika Msikiti Mkuu wa Qom na kuhudhuriwa na watu wa tabaka mbalimbali, alitaja hekima ya 147 kutoka katika "Nahjul Balagha", na kueleza kuwa: Katika hekima hii, Imam Ali (a.s) alimpa Kumail bin Ziyad nasaha zenye mwangaza na kanuni za kiakili na kimaadili na kusema: hotuba hii pekee ingekuwepo ndani ya "Nahjul Balagha", ingetosha kuthibitisha mwangaza, uongofu, na athari ya kitabu hicho kitukufu.

Aliweka msisitizo juu ya nafasi ya akili katika kuonesha njia sahihi, na kuongeza: Amirul-Mu’minin Ali (a.s) katika khutba hizi kwa hoja za kiakili alifafanua kuwa mwanadamu ni msafiri, na ili afikie malengo yake anahitaji njia na mwongozo. Malengo hayo yanaweza kuwa matamu au machungu, na kuchagua ni jukumu la msafiri mwenyewe kwa kuwa mwisho wa maisha ya kila mtu ni matokeo ya maisha yake ya Duniani. Hakuna nia, juhudi, wala kitendo kinachopotea. "Iwapo umevuna miiba, ni wewe uliyeipanda; na kama umefumua hariri, ni kwa mikono yako." Mtu akiishi kwa ujinga wa kielimu au wa kimatendo, basi amebeba miiba! Binadamu anapaswa kuishi kwa akili na elimu.

Amesema pia: Mtu akiiacha akili, maamuzi yake yatakuwa mabaya na maisha yake yatategemea mawazo ya kufikirika na udhanifu. Mtu wa aina hii anaitwa "mwenye kiburi" ndani ya Qur’ani, na mtu anayekatika maisha kwa mawazo bila kutumia akili si mpenzi wa Mwenyezi Mungu. Qur’ani inasema: "Hakika Mwenyezi Mungu hampendi kila mwenye majivuno ane jifaharisha." Kwa ajili hiyo, njia ya maisha ya mwanadamu inaweza kuwa ya kijinga ambayo ni upotovu; au ya kielimu ambayo ni njia ya wokovu japo si lengo la mwisho; na njia ya tatu ni ya "kugeuka na kukua" kuishi kwa elimu, busara, na matendo sahihi. Katika njia hii, uhusiano wa mtu na Mungu si wa mwalimu na mwanafunzi, bali wa mpenzi na mpendwa: "Yeye anawapenda wao, nao wanampenda Yeye." Uamuzi uko mikononi mwa mwanadamu mwenyewe.

Katika sehemu nyingine ya darsa hiyo, Ayatollah Jawadi Amoli alisisitiza umuhimu wa "heshima" katika umma wa kiislamu na kusema: Heshima kwa umma wa kiislamu haimaanishi kiburi, bali ni ishara ya haiba na nguvu ambayo inazuia maadui kuuvamia. Ikiwa jamii itafikiri kwa mujibu wa Qur’ani, badala ya kudhoofika na kuyumba, itapaswa kuonekana kwa heshima na nguvu.

Akinukuu aya za mwisho za Surah At-Tawbah, alisema: Mwenyezi Mungu anasema: "Enyi mlio amini! Piganeni na wale makafiri walio karibu yenu, na wakute ugumu kwenu." Maadui wenu lazima waogope uwepo wenu. Hili ni jambo la lazima, si la hiari. Umma wa kiislamu unapaswa kuwa na nguvu kiasi kwamba adui asiwe na ujasiri wa kuushambulia. Ni lazima wahisi ujasiri na ushujaa kutoka kwenu.

Akaongezea kuwa: Uwezo wa kuzuia uvamizi unapatikana kupitia haiba na muundo madhubuti wa ndani ya jamii. Haifai kuwa na ufisadi au vurugu ndani ya jamii ya kiislamu. Qur’ani si kwa ajili ya usiku wa ibada tu, bali ni kitabu hai kinachopaswa kutumika katika maisha ya kila siku ya Umma wa Kiislamu.

Akiweka mkazo juu ya historia na tamaduni ya Iran, alisema: Taifa la Iran ni taifa kubwa na lenye asili adhimu. Katika kila kona ya Iran kuna alama za elimu na ustaarabu. Wanazuoni wakubwa wa Qur’ani, wafasiri na waandishi wa vitabu vinne mashuhuri (kutub al-arba’ah) wametoka Iran. Nchi yetu leo ni mbeba bendera wa Ahlul Bayt duniani kote. Lazima tutambue ukubwa wetu na tusiuuze kwa thamani ndogo.

Katika hitimisho, Ayatollah Jawadi Amoli alisema: Qur’ani huifufua jamii. Lazima tuishi na Qur’ani, jamii ambayo Qur’ani ni msingi wake na aya zake zikapewa uhai na kufanyiwa kazi ipasavyo, basi jamii hiyo itasalia hai.

Maoni yako

You are replying to: .
captcha